MENENGAI CREAM WAZIDI KUTAMBA

Kocha mkuu wa Menengai Cream Cheetahs Lawi Buyachi ametaja ushindi wao wa Kenya Rugby Super Series kutokana na mipango mizuri na mpangilio mzuri kutoka kwa kikosi.
Mkufunzi huyo wa zamani wa Kisumu RFC na kocha msaidizi wa sasa wa Menengai Oilers aliongoza kikosi chake hadi kuibuka na ushindi baada ya kuichapa KCB Bank Lions 10-18 katika mechi yao ya mwisho iliyochezwa wikendi iliyopita katika uwanja wa RFUEA jijini Nairobi.
Lilikuwa taji la tatu la Super Series kwa Menengai Cream Cheetahs waliposhinda mechi tatu kati ya nne zilizochezwa katika msururu huo huku kichapo chao pekee kikitokea dhidi ya Faiba Mobile Rhinos.
Baada ya shindano la Rugby Super Series, timu sasa zinarejea kwenye Kombe la Enterprise ambalo lilikuwa limesitishwa ili kutoa nafasi ya kurejeshwa kwa Super Series ambayo ilikuwa imesimama kwa miaka kumi.
Imetayarishwa na Nelson Andati.