TUPO TAYARI KUMENYANA NA BURUNDI ASEMA KOCHA ALUOCH

Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 Ann Aluoch anasema kucheza na Burundi Jumapili nchini Ethiopia kutakuwa na manufaa katika kuhakikisha wanafuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la U17 la 2024.
Junior Starlets itaondoka nchini Ijumaa jioni kwa mechi ya raundi ya nne na ya mwisho ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia, ambayo itachezwa katika uwanja wa Abebe Bikila Stadium kutokana na kutopatikana kwa uwanja ulioidhinishwa na FIFA nchini Burundi.
Junior Starlets waliInga raundi ya mwisho baada ya kuwalaza Ethiopia mabao 3-0 usiku wa manane katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex, Nairobi.Junior Starlets walizidisha maandalizi yao mnamo Jumanne, Juni 4, 2024, katika uwanja wa Dandora kabla ya mechi ya mikondo miwili ya kufuzu dhidi ya Burundi. Walifungwa 1-2 na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) Kenya Police Bullets katika mechi ya kirafiki.
Mkondo wa kwanza wa mchujo utachezwa Jumapili, Juni 9, 2024 kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, huku mchezo wa marudiano ukipangwa. kwa wiki moja baadaye Juni 16, 2024 katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi. Mshindi wa jumla atawakilisha Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 17 mwaka wa 2024 nchini Jamhuri ya Dominika mwezi Oktoba, 2024.