WINCATE AJIUNGA NA SIMBA QUEENS
Mlinzi wa Harambee Starlets Wincate Kaari Kinyua amejiunga na miamba wa soka nchini Tanzania Simba Queens kwa mkataba wa miaka miwili kutoka klabu ya Yanga.
Kaari aliyewahi kuisakatia klabu ya ligi kuu ya soka nchini, Thika Queens, kabla ya timu hiyo kubadili jina na kujiita Kenya Police Bullets msimu jana, ataipiga jeki timu hiyo kuelekea taji la klabu bingwa afrika mashariki Cecafa linaloanza Agosti tarehe 17 jijini Addis Ababa Ethiopia na kutumika pia katika kufuzu kwa makala ya nne ya ligi klabu bingwa barani.
Kwenye ubingwa huo wa Cecafa, Simba imewekwa katika kundi B pamoja na PVP Buyenzi ya Burundi, Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FAD Djibouti ya Djibouti.
Kundi A linajumuisha mabingwa wa ligi kuu nchini kenya, Police Bullets, C.B.E ya Ethiopia, Yei Joint Stars ya Sudan Kaskazini, Warrior Queen ya Zanzibar na Rayon Sports Women ya Rwanda.
Selemani Makanya ni mratibu wa michezo klabuni Simba Queens aliyesifia ujio wa Kaari timuni humo na kusema utawapiga jeki pakubwa kuwania taji hilo la Cecafa.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 






































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































