MWANAMKE, WA MIAKA 32, AUAWA KATIKA SOKO LA DARAJA MBILI HUKO KISII

Polisi mjini Kisii wanachunguza kisa ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 32 amepatikana akiwa amefariki katika kijiji cha Mwamogesa Moraa katika Kaunti Ndogo ya Kitutu ya Kati.
Kulingana na polisi, marehemu kwa jina la Molly Achieng’, ambaye alikuwa akiishi katika kijiji jirani, amepatikana akiwa kwenye dimbwi la damu huku akiwa na majeraha kichwani na usoni.
Chifu Msaidizi wa eneo hilo Brian Otieno amesema marehemu alikuwa mfanyabiashara katika soko la Daraja Mbili na huenda alilengwa alipokuwa akifanya shughuli zake za kila siku.
Maafisa wa Polisi wametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za tukio hilo ili kuweza kuwakamata wahalifu na kuhakikisha wanafikishwa mahakamani.
Mwili wa marehemu umepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii kwa uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Imetayarishwa na Janice Marete