ADANI: ONYONKA AIBUA ‘USHAHIDI’ MPYA

Mkataba baina ya serikali na kampuni ya Adani unaendelea kuchukua mkondo mpya kila kuchao, wakati huu seneta wa Kisii Richard Onyonka akiibua ushahidi mpya kwamba licha ya kampuni 3 kuwasilisha mapendekezo ya kuukarabati uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA, mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege KAA ilipendelea kampuni ya Adani na kupuuza kampuni hizo.
Akizungumza katika bunge la seneti walipokuwa wakimhoji Waziri wa fedha John Mbadi, Onyonka amedai kwamba serikali ina njama ya kuficha maelezo muhimu kwenye mkataba huo, huku Waziri Mbadi akikanusha.
Hata hivyo, madai ya Onyonka yameibua mihemko wakati wa kikao hicho.
Aidha, maseneta Richard Onyonka, Edwin Sifuna na Samson Cherargei wameondoka kwenye kikao hicho baada ya kukosa kuridhishwa na majibu ya Mbadi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa