KENYA KUANDAA KONGAMANO LA KUKUZA SHUGHULI ZA BIASHARA ZINAZOZINGATIA HAKI ZA BINADAMU BARANI AFRIKA

Kongamano la tatu la Biashara na Haki za Kibinadamu barani Afrika limefunguliwa mjini Nairobi nchini Kenya, huku wajumbe wakitoa wito wa kuambatanishwa kanuni za usawa, haki na ushirikishwaji katika sekta binafsi barani humo.
Kongamano hilo lililoitishwa na muungano wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda, linafanyika chini ya kaulimbiu “Kukuza uwajibikaji wa biashara katika dunia inayobadilika kwa kasi.”
Zaidi ya washiriki 500, wakiwemo watunga sera, wasimamizi wa sekta, wanadiplomasia, wawakilishi wa wasomi na asasi za kiraia, wamehudhuria kongamano hilo ambalo limelenga kuhimiza mazungumzo na kujifunza kutumia mifano ya biashara inayoendeleza shughuli endelevu na za kimaadili.
Mwanasheria Mkuu wa Kenya Dorcas Oduor amesema bara la Afrika linazidi kutambua makutano muhimu kati ya shughuli za biashara na ulinzi wa haki za binadamu, akisisitiza kuwa Kenya ni nchi ya kwanza ya Afrika kuandaa mpango wa utekelezaji wa kitaifa kuhusu biashara na haki za binadamu.
Imetayarishwa na Mercy Asami