GOR MAHIA WAADHIBIWA NA BANDARI
Mechi ya Gor Mahia dhidi ya Bandari katika uwanja wa Ukunda Showground ilisitishwa mara mbili hapo jana baada ya mashabiki kuzua fujo dakika ya 80, muda mfupi baada ya Bandari kufunga bao lao la pili na kuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mwamuzi Kelvin Maina alisimamisha mchezo na kuwakusanya wachezaji katikati ya uwanja.
Baada ya kusimama kwa dakika 20, mchezo ulianza tena lakini muda si muda ulisimamishwa tena huku mvutano ukiendelea kuwa juu.
Hatimaye mechi hiyo ilichezwa dakika zilizosalia baada ya umati mkubwa wa mashabiki kuondoka uwanjani lakini hakuna bao lililoshuhudiwa tena na kuipa Bandari ushindi wa mabao 2-0 , mabao yaliyofungwa na Geoffrey Ojunga na Beja Nyamawi dakika ya 69 na 78 mtawalia.
Dakika ya 67, Kogalo walipunguzwa hadi wachezaji 10 baada ya nahodha Geoffrey Ochieng kumfanyia madhambi kijana Izzadin Ramadhan, nje ya eneo la 18.
Bandari wameendeleza msururu wao wa kutopoteza huku Gor Mahia ikipokea kichapo cha pili ndani ya siku 10.
Bandari ni ya nne na alama 11 huku Gor ikiwa ya 11 na alama 8 baada ya kucheza mechi 5 na mechi 6 mtawalia.
Kwengineko sofapaka walitupa uongozi wa bao moja dakika ya 8 kupitia kwa joseph kuloba na kuiruhusu Police Fc kusawazisha kupitia kwa David Okoth dakika ya 51 na kutoka sare 1-1.
Sofapaka ni ya 9 na alama 9 huku Pilice fc ikiwa ya 13 na alama 6.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































