BANDARI QUEENS WAICHARAZA MACMILLAN QUEENS 8-0

Bandari Queens FC waliwashangaza Macmillan Queens kwa kuwapiga mabao 8-0 katika mechi ya Women National Super League (WNSL) iliyochezwa kwenye uwanja wa Ukunda Showground, Kaunti ya Kwale, Jana Jumapili .
Bandari Queens waliwafariji mashabiki wao ambao walishuhudia timu ya wanaume ya Bandari FC ikishushwa hadhi na Bidco United kwa kichapo cha 0-2 kwenye uwanja huo huo mapema katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL).
Chilo Chikophe alifunga mabao matatu huku Agnes Olesi akipachika mawili na Happy Mutta, Tacy Olembo, na Salama Gaone wakifunga kila mmoja bao moja, na kufanikisha ushindi mkubwa. Olesi alifungua ukurasa wa mabao kwa timu ya wenyeji Bandari katika dakika ya pili tu baada ya kugonga mpira wa adhabu uliopigwa na Marion Wali huku walinzi wa Macmillan wakionekana kupotea.
Dakika nne baadaye, Chilo alipenya ngome yote ya Macmillan kabla ya kuachia shuti kali la chini lililompita kipa Irene Makungu.
Macmillan walirejea kwenye mchezo dakika za mwisho lakini juhudi kutoka kwa Diana Otieno na Lucy Nelina hazikufua dafu, na kipindi cha kwanza kilimalizika kwa mabao 2-0. Olembo alifunga bao la saba kwa shuti la yadi 30 lililotinga kwenye kona ya juu; kabla ya Gaone kumalizia ushindi huo katika dakika za nyongeza kwa pasi ya Irene Namale.
Kocha wa Bandari Queens, Janet Amunga, aliisifu timu yake kwa ushindi huo, akisema itarejesha hali ya kujiamini kwa wachezaji.
Imetayarishwa na Janice Marete