WATU WATANO WAFARIKI KATIKA AJALI HUKO MIGORI

Uchunguzi umeanzishwa na maafisa wa polisi baada ya watu watano, wakiwemo walimu wawili, kufariki papo hapo baada ya ajali iliyohusisha lori na pikipiki mbili katika daraja la Nyametembe, Kaunti ya Migori, usiku wa kuamkia leo
Mashuhuda wanasema lori lililokuwa likiendeshwa kwa kasi lilipoteza mwelekeo na kugonga waendesha pikipiki wawili waliokuwa na abiria, na kuwaua wote papo hapo. Kamanda wa Polisi wa Kuria Magharibi, Reuben Bett, amethibitisha kuwa waendesha pikipiki na abiria wao wamefariki, huku dereva wa lori akijeruhiwa na kulazwa hospitalini.
Bett ameongeza kusema kuwa lori lililokuwa likisafirisha mahindi lilipoteza udhibiti na kugongana na pikipiki zilizokuwa zikija upande wa pili.
Wakazi wa Nyametembe wamesema eneo hilo limekuwa hatari kwa ajali nyingi, wakitoa wito kwa Mamlaka ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) kupanua barabara na kuweka matuta ili kupunguza ajali.
Imetayarishwa na Janice Marete