KENYA YALENGA KUONGEZA MARA NNE MAUZO YA CHAI CHINA KUFIKIA 2030
Serikali ya Kenya imelenga kuongeza mara nne na zaidi mauzo ya chai nchini China ndani ya miaka sita ijayo. Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo na Mifugo, Mutahi Kagwe, ambaye amesema kuwa lengo ni kupandisha mauzo kutoka kilo milioni 12.42 mwaka huu wa 2024 hadi kufikia kilo milioni 50 ifikapo mwaka 2030.
Kagwe ametoa taarifa hiyo jijini Nairobi baada ya kikao na Zhang Chaobin, mwenyekiti wa kampuni ya chai ya Fuzhou Benny Tea Industry kutoka China. Mazungumzo hayo ni sehemu ya mikakati ya Kenya kupanua soko la chai kwenye taifa hilo la Asia na kuongeza ushawishi wake katika soko la kimataifa.
Waziri Kagwe amesisitiza kuwa China ni soko lenye fursa kubwa kwa chai ya Kenya, na serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa ili kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa wakulima wa chai nchini.
IImetayarishwa na Mercy Asami
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































