HESHIMA IDUMU KWA WANYAMA
Kocha mkuu wa Harambee Stars Benni McCarthy ametaka heshima idumishwe kwa nahodha wa zamani Victor Wanyama.
McCarthy anasema Wanyama ni nyota wa taifa ambaye ameiweka nchi kwenye ramani ya dunia kutokana na kuchezea baadhi ya vilabu maarufu duniani.
Wanyama aliitwa tena kwenye timu ya taifa wiki jana, kabla ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Chad nchini Morocco wiki hii.
Hata hivyo, uamuzi huo ulizua utata, huku baadhi ya jamii ya wanasoka nchini Kenya wakihisi kwamba kiungo huyo wa kati hana ubora kama wa zamani zake.
Tangu wakati huo, Wanyama amejiondoa katika timu ya taifa kutokana na shughuli za kibinafsi nchini Uingereza.
Akielezea uamuzi wake wa kumrejesha kwenye timu ya taifa-miaka minne baada ya Wanyama kustaafu-McCarthy alisema kujumuishwa kwake kutawasaidia wachezaji wachanga.
Harambee Stars itamenyana na Chad Alhamisi mjini Rabat kabla ya kukutana nao tena, wiki moja baadaye, katika uwanja huo huo.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































