WAKULIMA WAPINGA ADA YA KUSAFIRISHA KUKU KWA SH20 MACHAKOS
Muungano wa Wafugaji wa kuku Kenya (KPDA) umeibua wasiwasi kuhusu sheria mpya ya Kaunti ya Machakos ambayo imeweka ada ya Sh20 kwa kila kuku anayehamishwa kutoka kaunti hiyo, na kuonya kuwa uamuzi huo utaharibu ufugaji wa kuku na kulemaza maisha katika eneo lote.
Muungano huo, ambao unawakilisha wafugaji na wasindikaji wa kuku kote nchini, umeomba mkutano wa dharura na Gavana wa kaunti hiyo Wavinya Ndeti kujadili athari za sera hiyo mpya, ukielezea kuwa hilo litaleta vitisho kwa wakulima wanaofuga kuku katika eneo hilo.
Sekta ya kuku kote nchini inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji wadogo na tayari imekuwa ikikabiliana na kupanda kwa bei ya malisho, ongezeko la ushuru wa vifaa, na uagizaji wa bei nafuu kutoka nje. Kulingana na KPDA, ada ya ziada iliyowekwa na kaunti itazidisha hali hiyo, na kusukuma wakulima wengi kuzima shughuli zao za ufugaji wa kuku.
Muungano huo aidha umesisitiza kuwa ufugaji wa kuku unasalia kuwa uti wa mgongo wa maisha ya vijijini, hasa kwa wanawake na vijana, kutoa mapato muhimu kwa elimu, huduma za afya na mahitaji mengine ya kimsingi.
Imetayarishwa na Maurine Amwayi
English 











































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































