CITY WAWADHALILISHA WEKUNDU WA ANFIELD
Meneja wa klabu ya Manchester City Pep Guardiola aliadhimisha mechi yake ya 1,000 kama mkufunzi kwa mtindo wa aina yake, baada ya vijana wake kuwatia darasani wekundu wa Anfield Liverpool kwa kichapo cha mabao 3-0 ugani Etihad.
Kwenye mechi hiyo ambapo timu zote 2 zililenga kupunguza mwanya wa pointi na viongozi Arsenal, City walifanya ufungaji wa mabao kuonekana rahisi, Erling Haaland akianzisha adhabu katika dakika ya 29, baada ya awali mkwaju wake wa penalti kuokolewa na kipa wa Liverpool Giorgi Mamardashvili.
Hilo lilikuwa bao lake la kwanza dhidi ya Liverpool katika mechi ambapo beki wa Liverpool Virgil van Dijk alianzishwa.
Liverpool walipata mwanga katika kipindi cha kwanza kupitia Van Dijk, ila bao lake la kichwa kutokana na kona ya Mo Salah likafutiliwa mbali baada ya kuamuliwa kwamba Andy Robertson alikuwa katika eneo la offside na kumzuia kipa Gianluigi Donnarumma kuona mpira.
City walizidisha masaibu ya Liverpool ambao kwa kipindi kirefu walitatizwa na wing’a Jeremy Doku, kiungo Nico Gonzalez akivurumiza mpira wavuni dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza.
Baada ya kazi safi, Doku alifunga bao lake katika dakika ya 63, na kuwazima kabisa Liverpool ambao afueni yao, ni kwamba hawachezi na Man City kila wikendi.
Katika matokeo mengine, Chelsea waliandikisha ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wolves, mabao hayo yakipachikwa wavuni na Malo Gusto, Joao Pedro na Pedro Neto kwa faida ya Chelsea.
Kwingineko, viongozi Arsenal walishikwa katika sare ya magoli 2 na Sunderland, ambayo sasa ni timu ya kwanza kuifunga Arsenal bao baada ya mechi 8.
Manchester United pia waliandikisha sare ya magoli 2 dhidi ya Spurs.
Arsenal wanaelekea katika mapumziko wakiwa bado kileleni kwa pointi 26, 4 mbele ya Man City, Chelsea na Sunderland wakifunga 4 bora.
Bingwa mtetezi Liverpool sasa anashuka hadi nafasi ya 8 kwa pointi 18, pointi zinashikiliwa pia na Spurs, Manchester United, Aston Villa na Bournemouth.
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































