PSG YAILAZA BAYERN KUWEKA MIADI NA ARSENAL FAINALI
Mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa bara Ulaya, Paris St-Germain, watamenyana na viongozi wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza kwenye fainali ya kombe hilo, baada ya kuandikisha ushindi katika awamu ya semi fainali.
PSG waliilaza Bayern jumla ya mabao 6-5, licha ya sare ya bao 1-1 jana usiku kufuatia ushindi wa mabao 5-4 kwenye mkondo wa kwanza.
Wakiwa kifua mbele kabla ya mechi ya jana, mshindi wa tuzo ya Ballon d”Or Ousmane Dembele aliongeza uongozi wa PSG ndani ya muda wa dakika 3, baada ya kazi safi kutoka kwa wing’a wa Georgia Khvicha Kvaratskhelia.
Harry Kane aliyebanwa kwa kipindi kirefu na mabeki Marquinhos na Joao Neves, alifanikiwa kusawazisha katika dakika za majeruhi, ila wakabanduliwa kutokana na kichapo katika mkondo wa kwanza.
Kuelekea fainali, PSG watapigiwa upato kutetea ubingwa wao wa msimu jana wakilinganishwa na Arsenal, hasa kutokana na mchezo walioonyesha dhidi ya Bayern na katika fainali msimu jana ambako waliilaza Inter Milan mabao 5-0.
Miamba hao wa Ufaransa wanalenga kuwa timu ya pili tangu mwaka wa 1990, kutawazwa mabingwa kwa misimu miwili mfululizo, baada ya Real Madrid kufanikiwa kutetea ubingwa wao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 














































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































