#Football #Sports

LIGI YA MABINGWA ULAYA: USIKU WA MWISHO WA MAAMUZI

Kesho usiku ni siku ya mwisho ya hatua ya ligi ya UEFA Champions League, huku mvutano wa kujikatia tiketi ya moja kwa moja kwenda raundi ya 16 ukifikia kilele. Kwa mfumo mpya, timu nane za juu pekee ndizo zitafuzu moja kwa moja, huku zilizomaliza nafasi ya tisa hadi 24 zikilazimika kupitia mchujo wa play-offs.

Baadhi ya timu tayari ziko salama, lakini vigogo kadhaa wako ukingoni mwa nafasi nane bora na lazima washinde kesho.

Liverpool wanawakaribisha Qarabağ, na ushindi utawahakikishia kufuzu moja kwa moja. Sare nayo inaweza kuwatosha kulingana na matokeo mengine.

Tottenham Hotspur wako ugenini dhidi ya Eintracht Frankfurt, ushindi ukiwapeleka moja kwa moja raundi ya 16, lakini kupoteza au sare kunaweza kuwashusha hadi play-offs.

Newcastle United wanakabiliwa na mtihani mgumu ugenini dhidi ya bingwa PSG, na wanahitaji ushindi ili kuwa salama, la sivyo hatma yao itategemea matokeo ya timu nyingine.

Chelsea, nyumbani dhidi ya Napoli, nao wanahitaji pointi tatu ili kuepuka presha ya kuangalia tofauti ya mabao.

Kwa upande mwingine, Manchester City lazima waishinde Galatasaray na pia waombe matokeo mengine yawapendelee ili kuingia kwenye nafasi nane za juu.

Kwa mechi zote kuanza kwa wakati mmoja, kila bao litakuwa na maana kubwa, na mwisho wa filimbi ya mwisho, tutajua ni nani wanaokwenda moja kwa moja raundi ya 16 — na ni nani watalazimika kupitia njia ndefu ya play-offs.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *