MAHAKAMA YABATILISHA USHURU WA MAPISHI
Wakenya wanatazamiwa kunufaika na bei ya chini ya mafuta ya kupikia baada ya Mahakama Kuu kubatilisha uamuzi wa serikali wa kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa mafuta ghafi.Katika uamuzi wa Jaji Bahati Mwamuye, mahakama imetangaza ushuru huo kuwa kinyume na katiba, ikitaja ukosefu wa kibali cha bunge na ushirikishwaji wa maana wa umma.
Ushuru huo, ulioanzishwa Julai 2024 kupitia Tangazo la Gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulikuwa umechukua nafasi ya ushuru uliokadiriwa kuwa sifuri na kuchangia kupanda kwa bei ya mafuta ya kupika.Kulingana na watengenezaji, bei ya lita 20 ya mafuta ya kupikia iliongezeka kutoka takriban Ksh3,800 hadi Ksh4,200 baada ya kutozwa ushuru.
Watengenezaji pia walikuwa wametaja kupanda kwa gharama ya bidhaa kama vile majarini na sabuni. Bidhaa za vyakula kama vile chapati na mkate pia ziliathiriwa na ongezeko la bei ya mafuta ya kupikia.Kesi hiyo iliwasilishwa na Shirikisho la Wateja nchini (Cofek), ambalo lilidai kuwa ushuru huo ulitozwa bila mashauriano na kukiuka ulinzi wa kikatiba. Mahakama ilikubali, ikisema kwamba mamlaka ya ushuru yapo kwa Bunge na hayawezi kutekelezwa kwa upande mmoja na Watendaji au kupitia taratibu za kikanda.
Imetayarishwa na Maurine Amwayi
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































