ATHARI ZA UKAME KWA UZALISHAJI WA CHAI, MAPATO YA TAIFA
Uzalishaji wa chai nchini Kenya umeshuka kwa asilimia 13.55 katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2025, hali iliyochangiwa na ukame usio wa kawaida kulingana na Bodi ya Chai ya Kenya.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi hiyo, Willy Mutai, amesema kwenye taarifa iliyotolewa jijini Nairobi kwamba uzalishaji kwa kipindi hicho ulikuwa kilo milioni 98.9, ikilinganishwa na kilo milioni 114.4 katika kipindi sawa cha mwaka jana.
Mwezi ulioathirika zaidi ulikuwa Februari, ambapo uzalishaji ulikuwa kilo milioni 44, upungufu wa kilo milioni 10.8 ikilinganishwa na mwezi Februari wa mwaka 2024.
Vilevile, amesema kuwa ukame uliathiri pakubwa uzalishaji wa chai mwezi Februari, ambapo mashariki mwa Bonde la Ufa kulishuhudiwa kushuka kwa asilimia 21, huku magharibi ikishuka kwa asilimia 18.6.
Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Mamlaka ya Maendeleo ya Kanda ya IGAD kimetabiri kuwa Kenya itapokea mvua chini ya wastani katika msimu wa mvua wa Machi hadi Mei, hali ambayo huenda ikaathiri zaidi uzalishaji wa chai mwaka huu.
Chai ni mojawapo ya mazao makuu ya kigeni yanayoingiza mapato nchini Kenya, sambamba na utalii na maua.
Imetayarishwa na Mercy Asami
English 




















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































