EZE AIPA ARSENAL HATAMU, BRENTFORD IKIZIDISHA MASAIBU ANFIELD
Kiungo wa Arsenal Eberechi Eze aliifungia Arsenal bao lake kwanza la msimu tangu kuigura klabu ya Crystal Palace, na kuihakikishia Arsenal ushindi mwembamba na muhimu wa bao 1:0 dhidi ya klabu hiyo.
Ushindi wa Arsenal umeimarisha uongozi wao wa ligi kuu ya Uingereza, hasa baada ya washindani wao Chelsea, Manchester City na bingwa mtetezi Liverpool kupoteza mechi zao.
Ugani Old Trafford, Manchester United waliandikisha ushindi wao wa mechi 3 mfululizo walipoikalifisha Brighton kwa kibano cha mabao 4-2, Matheus Cunha akifungua mifereji ya magoli kwa United kabla ya Casemiro, na Bryan Mbeumo kufuata nyao.
Mchezaji wa zamani wa United Danny Welbeck na Charalampos Kostouls waliipa United shinikizo, ila mabao yao haikuwawezesha kupata pointi.
Wakati uo huo, msusuru wa matokeo duni uliendelea Anfield, baada ya Liverpool kucharazwa na mabao 3-2 na Brentford, hii ikiwa ni mechi yao ya 4 mfululizo kupoteza katika ligi.
Manchester City pia walitamatisha rekodi yao ya mechi 9 bila kupoteza, baada ya kuzabwa bao 1-0 na Aston Villa, bao la Matt Cash likitia doa vijana wa Pep Guardiola ambao wamekuwa katika fomu ya aina yake.
Kwingineko, Chelsea walitiwa darasani na Sunderland, ambao walibomoa daraja la Stamford kwa mabao 2-1, matokeo ambayo yameendelea kuibua maswali kuhusu mwelekeo wa Chelsea.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 











































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































