SUDAN YASHINDA

Sudan ilishinda kikwazo cha kutocheza nyumbani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kuishinda Niger 1-0 katika mechi ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025.
Sudan ilikuwa mwenyeji wa Niger mjini Juba, mji mkuu wa nchi jirani ya Sudan Kusini, na bao la dakika ya 51 kutoka kwa Abo Eisa mwenye kucheza soka la malipo nchini Thailand liliipatia nchi yake pointi tatu Kundi F.
Mapigano kati ya jeshi la taifa na kikosi cha wanamgambo nchini Sudan yalizuka mnamo Aprili 2023, na kulazimisha timu ya taifa kufanya mazoezi na kucheza nje ya nchi tangu wakati huo.
Katika mechi nyingine, Comoro ilitoka sare ya 1-1 na Gambia, huku Rwanda ikipata matokeo sawa na hayo dhidi ya wenyeji Libya katika Kundi D, Ethiopia ikiwazuia wenyeji Tanzania 0-0 jijini Dar es Salaam, mchezo wa Kundi H.
Kuna mechi saba za kufuzu zilizopangwa kufanyika leo.
Imetayarishwa na Nelson Andati