KQ YAZINDUA SAFARI ZA NDEGE KUTOKA NAIROBI – MSUMBIJI

Shirika la Ndege la Kenya (KQ) limeanza tena safari za ndege za moja kwa moja kati ya Nairobi na Maputo ya Msumbiji ili kusaidia kuimarisha mawasiliano ya ndani ya Afrika.
KQ imesema safari hizo tatu za ndege kila wiki, Jumatano, Ijumaa, na Jumapili, zitahudumia wasafiri wanaotoka Kenya na zitatumika kama njia rahisi ya kuunganisha abiria kutoka miji mingine ya Afrika kupitia Nairobi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Ndege la KQ, Allan Kilavuka amesema kuzinduliwa upya kwa safari hizo ni udhihirisho wa wazi wa maendeleo ya shirika hilo na mustakabali mzuri.
Ameongeza kuwa kuzinduliwa kwa njia ya 45 ya shirika hilo ya kwenda Maputo, kunaashiria hatua muhimu ya kampuni hiyo kupanua huduma zake.
Imetayarishwa na Janice Marete