#Business

SENETI YAJADILI MSWADA WA KUDHIBITI BIASHARA YA BODA BODA

Mswada unaonuiwa kudhibiti matumizi ya pikipiki (bodaboda) nchini sasa uko mbele ya Seneti.
Mswada huo unalenga kuwasilisha masharti mapya ya usajili na uendeshaji wa pikipiki zinazotumiwa katika uchukuzi wa umma na usalama wao katika ngazi ya kaunti.

Iwapo utaidhinishwa, Mswada huo unaofadhiliwa na Mnadhimu Mkuu wa Wengi katika Seneti Boni Khalwale utatoa fursa ya usajili wa waendesha bodaboda na kutambuliwa na bodi husika katika kila kaunti.

Mswada huo sasa katika hatua ya pili ya kusomwa, unaeleza kuwa mtu hataendesha bodaboda isipokuwa amemaliza mafunzo ambayo yanajumuisha mbinu za uendeshaji salama na za kujihami, sheria na kanuni za barabarani, matunzo na adabu kwa wateja, utunzaji wa dharura, matengenezo ya msingi ya pikipiki na ufahamu wa usalama.

Khalwale anataka kila mmiliki wa Bodaboda kuwapa waendeshaji kofia mbili ambazo zinatii viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango la Kenya na ni za rangi iliyoainishwa na jaketi mbili za kuakisi, pia za rangi maalum.

Mswada unalenga kuwa kila mpanda pikipiki awe na cheti cha usajili na kuhakikisha kwamba hatambeba mtu kwenye pikipiki bila vifaa vya kujikinga vilivyowekwa vyema.

Imetayarishwa na Janice Marete

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *