#Football #Sports

ARSENAL WAJIOKOA DHIDI YA SPURS, CITY WAKIMBIZA

Kiungo wa Arsenal Eberechi Eze aliwahangaisha Tottenham mara tena tangu kujiunga na Arsenal, akifunga mabao 2 kwenye ushindi wa mabao 4-1 kwenye debi la London jana na kuwarejeshea Gunners uongozi wa pointi 5.

Maangamizi mengine yalitekelezwa na Viktor Gyokeres ambaye pia alifunga mara 2, na kuzima juhudi za Kolo Muani kujaribu kuwarejesha Spurs mchezoni.

Ushindi wa vijana hao wa Mikel Arteta ulitamatisha kipindi cha mechi 2 bila ushindi, na kuwazima wakosoaji.

Baada ya kukatalia mbali ofa ya kujiunga na Spurs na kukubali kujiunga na Arsenal, Eze amewafunga Spurs mabao 5 katika mechi 2 walizokutana, akipachika hattrick katika mechi ya mkondo wa kwanza wa ligi kuu ya EPL Novemba mwaka jana.

Eze na Gyokeres ambao wamekuwa na msimu mgumu tangu kuwasili kutoka Palace na Sporting CP mtawalia, walionyesha kuimarika kwao wakati muhimu ambao Arsenal walionekana kuyumba kipute cha EPL kinapoelekea tamati.

Ushindi huo umewasukuma hadi pointi 61 baada ya mechi 28, pointi 5 mbele ya Manchester City ambao wana mechi moja mkononi.

Mechi ya jana ilikuwa na shinikizo, hasa kufuatia ushindi wa mabao 2-1 wa City dhidi ya Newcastle.

Utovu wa nidhamu uliwaponza Chelsea mara tena, wakitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Burnley baada ya Wesley Fofana kuonyeshwa kadi nyekundu Chelsea walipokuwa kileleni.

Leo ni zamu ya Manchester United ambao watakuwa wageni wa Everton kwenye mechi nyingine ya EPL.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *