PAMBANO LA GOR- BANDARI LAHAMISHWA
Mchuano wa ligi kuu ya soka KPL kati ya viongozi wa ligi hiyo Gor Mahia na Bandari FC utachezewa katika uwanja wa michezo wa Kwale tarehe 12 mwezi huu, na wala si uwanja wa nyumbani wa Bandari wa Mbaraki.
Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa Bandari FC Tony Kibwana, hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wakati wa mechi hiyo na kuudhibiti umati, akisema wanatarajia mashabiki wengi kutokana na msimu wa sherehe.
Shirikisho la soka nchini FKF maajuzi liliidhinisha uwanja wa michezo wa Kwale kuwa mwenyeji wa michuano ya ligi kuu.
Aidha, Kibwana amesema uwanja huo utakuwa wa nyumbani kwa mechi za wanaforodha hao kuanzia mwishoni mwa Januari mwaka ujao.
Kabla ya mchuano huo, Bandari ambao wamekuwa na msimu mgumu wakiandikisha ushindi mara 2 pekee, watamenyana na APS Bomet ugenini wikendi hii, nao Gor Mahia wakiwa mwenyeji wa Murang’a.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































