POLICE FC WATAWAZWA MABINGWA KPL
Klabu ya Police FC imejikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa barani Afrika msimu ujao baada ya kutawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Kenya KPL hapo jana.
Police waliochukua taji hilo kwa mara ya kwanza wiki moja iliyopita, wametawazwa rasmi hapo jana kwenye mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya mabingwa wanaondoka Gor Mahia katika uwanja wa Ulinzi Complex, mechi iliyotamatika katika sare ya bao 1.
Mechi hiyo iliyoshuhudia Gor kuwawekea maafande gwaride la heshima, ilihudhuriwa na viongozi mashuhuri nchini akiwemo kinara wa ODM Raila Odinga, ambaye alipewa jukumu la kuikabidhi Police FC taji hilo ambalo ni jipya.
Kwenye matokeo mengine, FC Talanta na Nairobi City Stars walishushwa daraja baada ya kumaliza mkiani kwenye msimamo wa Ligi, Talanta wakitandikwa bao moja bila mikononi mwa Murang’a Seal huku City Stars wakitoa sare ya kutofungana dhidi ya Mathare United kwenye siku ambapo timu 6 zilikuwa zikiwania kuepuka kushushwa daraja.
Talanta na City Stars walimaliza msimu wakiwa na pointi 35, sawa na Posta rangers na Bidco United waliomaliza katika nafasi za 16 na 15 mtawalia, Posta na Talanta wakifanana kwa kila kitu ukiwemo utofauti wa mabao waliofunga na kufungwa, ila Posta wakawa juu ya Talanta kutokana na matokeo ya mechi baina yao msimu huu ambapo Posta iliwashinda Talanta mabao 2:1 baada ya sare ya 0 katika awamu ya kwanza.
Imetayrishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































