MBOGA ZAKATAA KUSHUKA

Wakenya wanaendelea kugharamika pakubwa katika ununuzi wa mboga, licha ya kushuka kwa bidhaa nyingi za matumizi ya nyumbani kiujumla.
Katika mwezi wa Julai, bei ya kabeji, nyanya na vitunguu ilipanda kwa kasi ila kukawa na kushuka kwa bei za bidhaa nyinginek ama vile mahindi na mchele hali iliyosababisha mfumuko wa bei kushuka hadi asilimia 4.3.
Kilo moja ya nyanya iliongezeka kwa asilimia 28.7 hadi Shilingi 98 Julai mwaka huu kutoka Shilingi 76.7 katika kipindi kama hicho mwaka jana. Wapenzi wa kachumbari sasa watalazimika kuchimba zaidi mifukoni mwao huku bei ya vitunguu ikiongezeka kutoka Shilingi 129.79 hadi shilingi 171.41 kwa kilo moja ya bidhaa hiyo katika kipindi hicho.
Bei ya kabeji ilirekodi ongezeko kubwa la bei kutoka Shilingi 53.7 hadi Shilingi 78.4 kwa kilo moja ya bidhaa hiyo. Hili lilikuwa ni ongezeko la asilimia 46.1. Hata hivyo, kulingana na KNBS, bidhaa za matumizi ya nyumbani nchini zilipata nafuu ya gharama ya bidhaa mbalimbali za vyakula, huku bei ya sukari ikishuka kwa asilimia 22.3 mwaka hadi Shilingi 164.42 kwa kilo moja.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa