KENYA KUTUMIA MAENEO MAALUM YA KIUCHUMI KUONGEZA MAUZO YA NJE
Katibu Mkuu katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda Abubakar Hassan Abubakar amesema serikali kuu inapanga kutumia maeneo maalum ya kiuchumi ili kuimarisha msingi wa viwanda na kuongeza mauzo ya nje.
Abubakar ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Kifaru Exim yaliyoko katika Tatu City, akiongeza kuwa Kenya imetenga maeneo maalum ya kiuchumi yanayomilikiwa na umma na watu binafsi ambayo yanatoa motisha za kifedha na kiutawala kwa wawekezaji wa ndani na nje. Maeneo hayo yana fursa ya kutoa jukwaa la ongezeko la thamani la kupanua uzalishaji katika sekta ya kilimo, dawa na nguo.
Amebainisha kuwa maeneo hayo kama vitovu shindani vya utengenezaji, yataiwezesha Kenya kupata mikataba mingi ya upendeleo ya kibiashara inayosainiwa na washirika wa kibiashara ili kukuza mauzo ya nje.
Mkuu wa idara ya huduma za maendeleo ya biashara katika Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi Victor Mageto amesema kuwa Kenya inatekeleza mageuzi ili kurekebisha kanuni na kupunguza vikwazo vya ukiritimba pamoja na gharama ya kufanya biashara.
Imetayarishwa na Maurine Amwai
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































