MATUMAINI YA KNUT YA KUFIKIA MAKUBALIANO NA TSC

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Collins Oyuu, amewahakikishia walimu kuwa mazungumzo yao na Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kuhusu Mkataba wa Pamoja wa Makubaliano (CBA) yanaendelea vizuri.
Oyuu, akizungumza mjini Rongo, Kaunti ya Migori, amesema maafisa wa chama wamekuwa na mikutano kadhaa na TSC.
Akieleza matumaini kwamba mahitaji ya walimu yatatimizwa hivi karibuni na TSC.
Miongoni mwa masuala ambayo KNUT inashinikiza katika mazungumzo hayo ni kupandishwa vyeo kwa walimu ambao wamekwama katika kundi moja la kazi kwa miaka mingi.
Kulingana na Oyuu, TSC imefichua kuwa imepokea shilingi bilioni 1.1 pekee kwa ajili ya kupandisha vyeo, ambayo haitoshi kupandisha vyeo walimu wote wanaostahili.
Oyuu aidha ameongeza kuwa wanashinikiza kutengwa kwa fedha zaidi ili walimu wote wanaostahili kupandishwa vyeo waweze kupandishwa huku akibainisha kuwa suala la kupandishwa vyeo kwa walimu ni changamoto kubwa nchini ambayo lazima serikali ishughulikie kwa wakati ufaao.
Wakati huohuo, ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono Mtaala wa umilisi (CBC) akisema mtaala huo mpya una changamoto ila zinaweza kushughulikiwa na wadau wote kwa msaada wa fedha kutoka serikalini.
Imetayarishwa na Janice Marete