“NAIROBI UNITED JOGOO LA SHAMBA”
Masaibu ya klabu ya Nairobi United barani Afrika yaliendelea hapo jana katika mechi yao ya mashirikisho yaani CAF Confederations Cup, baada ya kurambishwa kichapo cha 5 mfululizo katika mechi za makundi, mara hii wakidhalilishwa nyumbani na miamba wa Morocco Wydad AC baada yao kupoteza nafasi nyingi.
Bao la Wissam Ben Yedder katika dakika za majeruhi liliipa Wydad ushindi mwembamba wa bao 1-0, na pointi 3 nono zilizowahakikishia udhabiti katika uongozi wa Group B.
Naibois walianza mechi hiyo kwa kishindo wakilenga kupata angalau pointi moja katika awamu ya makundi licha ya kuwa tayari wamebanduliwa, beki Shami Mwinyi akipoteza nafasi 2 za wazi katika kipindi cha kwanza, nalo bao la Dancan Omalla likifutiliwa mbali kutokana na offside.
Hatari ya pekee ambayo wageni walionyesha katika kipindi cha kwanza ilikuwa kupitia kwa kiungo wa zamani wa Chelsea Hakim Ziyech, ila shuti lake likapaa angani.
Naibois wakionekana kuambuliwa sare na pointi yao kwanza, nguvu mpya Yedder alizima matumaini hayo, sasa wakisalia na mechi ya mwisho dhidi ya Maniema Union ya DR Congo wikendi ijayo.
Maniema wataingia mechi hiyo wakilenga ushindi huku wakiomba Wydad iwashikie Azam, baada ya miamba hao wa Kongo kuzimwa kwa bao 1-0 na Azam, wote sasa wakiwa na pointi 9 huku Wydad wakiwa na pointi 12.
Timu 2 za kwanza katika kila Kundi zitafuzu awamu ya robo fainali.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































