BAYERN MUNICH WAONJESHWA KICHAPO CHA KWANZA
Miamba wa soka nchini Ujerumani Bayern Munich walionja kichapo cha kwanza cha msimu baada ya kupeperushwa ugani Fly Emirates na wenyeji Arsenal, na kupokezwa kichapo cha mabao 3-1 katika kinyang’anyiro cha klabu bingwa bara Ulaya.
Jurien Timber alianzisha matatizo kwa vijana wa Vincent Kompany kunako dakika ya 22 kupitia kichwa kutokana na kona kiki yake Bukayo Saka, akijitwika mpira na kuujaza wavuni.
Lennart Karl aliwarejesha Bayern Mchezoni na kufanya mambo kuwa sare kuelekea mapumzikoni, ila adhabu zaidi ikashuka dhidi ya miamba hao.
Noni Madueke aliwarejeshea Arsenal uongozi, likiwa bao lake la kwanza tangu kujiunga na klabu hiyo, naye Gabriel Martinelli ambaye amepewa jina la Finisher na kocha Mikel Arteta, kumalizia mchezo katika dakika ya 77 kutoka kwa pasi ya shujaa wa wikendi iliyopita Eberechi Eze.
Arsenal sasa ndiyo timu ya pekee ambayo haijapoteza mechi katika dimba hilo msimu huu, wakiwa na kileleni kwa pointi 15 kutokana na mechi 5.
Katika matokeo mengine, masaibu ya wekundu wa Anfield Liverpool katika ligi zote yaliendelea, wakizimwa nyumbani kwa kibano cha mabao 4-1 na PSV Eindhoven.
Mabingwa hao wa Uingereza walitiwa kikaangoni na kupakuliwa katika dakika ya 6, Ivan Perisic akifunga kupitia mkwaju wa penalt.
Wing’a wa Hungary Dominik Szoboszlai alisawazisha dakika 10 baadaye, ila bao lake likasalia kuwafuta machozi vijana wa Arne Slot.
Kichapo hicho kinawashusha Liverpool hadi nafasi ya 13 kwenye jedwali la timu 32.
Timu 8 za kwanza zitafuzu awamu ya 16 bora moja kwa moja, nambari 9 hadi 24 zikishiriki mwondoano ili kupata 8 kati yazo kuingia awamu hiyo.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































