#Football #Sports

ARSENAL YAKARIBIA TAJI EPL, CITY WAYUMBA

Timu ya Arsenal imekaribia ubingwa wa taji la ligi kuu ya soka nchini Uingereza, EPL, kufuatia ushindi wao mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Brighton ugani Amex, huku wapinzani wao wa karibu Manchester City wakidondosha pointi 2 muhimu, walipoandikisha sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Nottingham Forest.

Katika mtindo wa ubingwa, Bukayo Saka aliwapa Gunners bao la uongozi katika dakika za ufunguzi kwenye mechi yake ya 300 kwa vijana hao wa Mikel Arteta, ambalo mwishowe liliwapa pointi 3 muhimu na kuwasukuma mbele ya City kwa pointi 7.

Kwa kipindi kirefu, mechi hiyo ilikosa ladha kutokana na kusimamishwa mara kwa mara wachezaji wa Arsenal walipodai kujeruhiwa, hatua ambayo imekosolewa vikali na mkufunzi wa Brighton, Fabian Hurzeler.

Manchester City, wake Pep Guardiola walio katika nafasi ya pili na mechi moja mkononi, walionekana kuwa kwenye mkondo wa kupata ushindi rahisi dhidi ya wageni wao wanaokabiliwa na hatari ya kushushwa daraja.

City walimiliki asilimia kubwa ya mchezo na kubuni nafasi ya nyingi za kufunga mabao ila wakashindwa kuzitumia, sajili wa Januari Antoine Semenyo akifunga moja kati ya nafasi hizo za kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, licha ya City kudhibiti mchezo, Forest walitoka nyuma mara 2 kulazimimisha sare hiyo, na kuwapa pointi ambayo imewaondoa kwenye eneo la hatari kwa ubora wa mabao juu ya West Ham United.

Katika matokeo mengine, Manchester United waliokuwa wamesahau jinsi ya kupoteza mechi, walikumbushwa kwamba kurudi nyuma si kazi, walipocharazwa mabao 2-1 na Newcastle United na kumkabidhi Michael Carrick kichapo chake cha kwanza.

Licha ya Newcastle kusalia wachezaji 10 kufuatia kadi nyekundu kwa kiungo wao Jacob Ramsey, William Osula aliwalemea mabeki wa United na kufunga bao la ushindi katika dakika ya 90, baada ya bao la Casemiro awali kufuta bao la ufunguzi la Newcastle kupitia Anthony Gordon.

Na katika kinyang’anyiro kingine cha kuwania kushiriki dimba la klabu bingwa bara Ulaya msimu ujao, Chelsea waliandikisha ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Aston Villa, kufuatia hattrick yake Joao Pedro ambayo iliwashusha Liverpool hadi nafasi ya 6.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

ARSENAL YAKARIBIA TAJI EPL, CITY WAYUMBA

HISA ZA UUZAJI WA KPC ZILIIPA KENYA

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *