MIHESO AFUNGA MIKOBA KUTOKA LEOPARDS
Nahodha na kiungo mkongwe wa AFC Leopards Clifton Miheso ametangaza rasmi kuachana na klabu hiyo baada ya kumalizika kwa mkataba wake, na hivyo kuashiria mwisho wa ukurasa muhimu kwa mmoja wa wanasoka wenye uzoefu zaidi nchini Kenya.
Katika ujumbe mzito uliotumwa kwenye mitandao yake ya kijamii, Miheso aliwashukuru mashabiki, wachezaji wenzake, na kocha wa zamani Thomas Trucha kwa usaidizi wao usioyumba wakati wote wa uongozi wake.
Miheso, ambaye alijiunga na Ingwe mara kadhaa katika muongo mmoja uliopita, anaacha historia ya uongozi na uzoefu.
Kuondoka kwake ni sehemu ya mabadiliko makubwa katika dimba la Den, huku winga Elly Wafula, mshambuliaji Sydney Lokale, kipa Abubakar Musha, na kiungo mkongwe Kevin Kimani pia wakiondoka katika klabu hiyo.
Huku AFC Leopards ikitazamia kujijenga upya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya FKF, kuondoka kwa wachezaji hao wa kitambo kunaashiria mwanzo mpya, uliojaa hali ya sintofahamu lakini pia kuahidi.Klabu hii inatoka katika kampeni ya kutamausha, ikimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa KPL kwa alama 51.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































