MARTHA AMUNYOLET ALENGE KIATU CHA DHAHABU
Mshambulizi wa Harambee Starlets, Martha Amunyolet analenga kiatu cha dhahabu katika michuano ya Kombe la CECAFA ya Wanawake inayoendelea nchini Tanzania.
Amunyolet ameifungia timu hiyo mabao matatu katika mechi mbili za kwanza dhidi ya Burundi na Uganda.
Kando na kusaidia timu kuinua gongo, Amunyolet anasema itakuwa furaha maradufu ikiwa pia angeshinda tuzo ya mfungaji bora.
“Nataka katika mechi zote mbili dhidi ya Burundi na Uganda, nililenga kufunga mabao na nilifanikiwa. Mechi hizo mbili zimekuwa nzuri kwetu lakini hatuwezi kusema zimekuwa rahisi. Tulicheza kwa kujitolea. Nina furaha tulifunga bao la kuridhisha.
“Tumekuwa tukitoa kila kitu kufika hapa licha ya kwamba upinzani ni mgumu,” alisema Amunyolet.
Starlets watakuwa wakipania kupata ushindi mwingine watakapomenyana na Sudan Kusini bila ushindi siku ya Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 4:00 usiku.
Starlets wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa na ushindi mkubwa mara mbili mfululizo dhidi ya Burundi, ambao waliwazaba 3-0 na kuwabomoa Uganda 4-0 na kufikisha pointi sita.
Wenyeji Tanzania pia wana pointi sita, lakini wanafurahia tofauti ya mabao.
Sudan Kusini kwa upande mwingine, ilipoteza mechi zake mbili za ufunguzi, 4-0 na Tanzania na 5-0 na Uganda.
Imetayrishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































