GOR WATAMBA MBELE YA SERIKALI
Washikilizi wa rekodi ya ubingwa wa ligi kuu nchini KPL Gor Mahia, walichukua uongozi wa ligi hiyo hapo jana baada ya kutamba mbele ya Serikali walipowacharaza mabingwa watetezi Police FC kibano cha mabao 2-0 ugani Nyayo.
Pambano hilo lililokuwa limepewa jina la Sirkal Derby, lilitarajiwa kutifua kivumbi ila likageuka fedhaha kwa maafande, ambao ni maajuzi tu walibanduliwa nje ya kipute cha klabu bingwa barani Afrika.
Felix Oluoch aliwaweka Gor mbele baada ya kumegewa pasi na raia wa Ghana Ebenezer Adu-Kwaw, Musa Sharif akiweka msumari wa mwisho kwenye bendera kunako dakika ya 33.
Ushindi huo unawainua Green Army hadi kileleni kwa pointi 16, 2 mbele ya Kakamega Homeboyz.
Katika mechi nyingine, APS Bomet waliandikisha sare ya pili mfululizo kufuatia sare ya goli 1 dhidi ya Mathare United, matokeo sawa yakishuhudiwa kwenye mechi baina ya Bandari FC na KCB FC, kabla ya wanajeshi wa Ulinzi kulishwa matoke na Shabana FC walioandikisha ushindi wa goli 1-0.
Ingwe walirambishwa sukari mara 2 bila kutoa kucha na Mara Sugar Jumamosi, matokeo ambayo yanawaacha katika nafasi ya 4, nao Nairobi United wakirejea kwa kishindo na kupanda hadi nafasi ya 3 kufuatia ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Kariobangi Sharks.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































