JERAHA LILINIKOSESHA KIATU CHA DHAHABU

Mshambulizi wa Bungoma Queens, Catherine Khaemba anadai alikosa Kiatu cha Dhahabu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya FKF 2024/25 kutokana na jeraha.
Khaemba alikuwa akiongoza orodha ya wafungaji katika mkondo wa kwanza wa ligi kabla ya kukosekana kwa sababu ya jeraha la mguu, ambalo lilitoa fursa kwa fowadi wa Police Bullets, Rebecca Okwaro na mshambuliaji wa Kibera Soccer Women, Faith Mboya kutinga nafasi mbili za juu katika mbio za wafungaji bora.
Okwaro wa mabingwa Kenya Police Bullets aliongoza chati ya wafungaji kwa mabao 16, akifuatiwa na Faith Mboya wa Kibera Soccer Women aliyefunga mabao 15, huku Catherine Khaemba akimaliza wa tatu kwa mabao 13. Wakati huo huo, fowadi huyo ameahidi kujiandaa vilivyo kabla ya msimu ujao na kuwahakikishia mashabiki wa Bungoma Queens kwamba ataongoza chati ya wafungaji.
Imetayarishwa na Nelson Andati