ARSENAL YAPUNGUZA MWANYA, UTOVU WA NIDHAMU WABOMOA DARAJA
Klabu ya Arsenal ililazimisha ushindi wa mabao 2:1 dhidi ya Newcastle dakika za lala salama, baada ya kuwa nyuma kuanzia kipindi cha kwanza kufuatia bao la kichwa la Nick Woltemade katika dakika ya 34.
Mabao kutoka kwa Mikel Merino na Gabriel Magalhaes yalihakikisha kuwa the Gunners wanapunguza mwanya wa alama kati yao na vigogo Liverpool, ambao walionja kipigo cha kwanza cha msimu kwa kutandikiwa mabao 2:1 na Crystal Palace Jumamosi.
Arsenal walionekana kupoteza nafasi ya kipekee kuwakaribia the Reds, watatumia ushindi wa hapo jana kujiimarisha, kwa matumaini ya kunyakua ubingwa wa EPL msimu huu baada ya majaribio kwa zaidi ya miaka 20.
Wakati uo huo, kocha mkuu wa Manchester United Ruben Amorim amesema katu hatajitetea aua hata kuwatetea wachezaji wake dhidi ya shinikizo zonazoendelea kutolewa, hasa kufuatia kibano cha mabao 3:1 mikononi mwa Brentford.
Kipigo mara 3 katika mechi 6 za ufunguzi wa ligi kimemmwacha Amorim akikabiliwa na uwezekano wa kutimuliwa, maswali yakiibuliwa kuhusu safu yake ya ulinzi iliyoonyesha kufuja kwa hali ya juu kwenye mechi ya Jumamosi, mashabiki wakianza kuimba nyimbo za kumtishia kwamba angefutwa jana asubuhi.
Licha ya Benjamin Sesko kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na United mapema msimu huu kutoka RB Leigpzig, masaibu ya United yaliongezeka wakati kiungo Bruno Fernandez alipoteza mkwaju wa penalti uliopanguliwa na kipa Caoimhin Kelleher.
Huku hayo yakijiri, utovu wa nidhamu umeendelea kuiponza Chelsea ambao walipata kadi nyekundu katika mechi 2 mtawalia.
Beki Trevor Chalobah alionyesha kadi hiyo Jumamosi katika mechi dhidi ya Brighton ambao waliwadhalilisha The Blues kwa kibano cha mabao 3:1, kikiwa kibano cha pili mtawalia huku wakimaliza wakiwa wachezaji 10.
Baada ya mechi 6, Liverpool wangali kileleni kwa alama 15, Arsenal wakishikilia nafasi ya 2 kwa alama 13, Crystal Palace wakiwa wa 3 kwa alama 12 kufuatia ushindi dhidi ya Liverpool.
Manchester City wamepanda hadi nafasi ya 7 kwa alama 10 kufuatia ushindi wa mabao 5:1 dhidi ya Burnley, nao Chelsea wakishuka hadi nafasi ya 8 kwa alama 8, alama 7 kutoka kwa viongozi.
United sasa wamo katika nafasi ya 14 kwa alama 7 pekee katika mechi 6.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 


























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































