MWANIKI ATOLEWA NJE

Mwendesha baiskeli Benson Mwaniki ameondolewa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris 2024, baada ya kuvunjika bega na uti wa mgongo katika ajali mbaya wiki iliyopita.
Mwaniki, ambaye alikuwa rubani wa mwendesha baiskeli Kennedy Ogada, anahitaji angalau wiki sita kupata nafuu baada ya kuangushwa na gari walipokuwa wakienda mazoezini huko Compiegne, Ufaransa.
Hata hivyo, Ogada, ambaye hakujeruhiwa bado yumo katika ubora wake na ameahidi kujizatiti na kuvuna medali endapo atapata rubani mwingine kwa wakati mzuri, licha ya misukosuko.
Kiongozi wa ujumbe wa kikosi cha Kenya Dennis Muga alisema Kamati ya Kitaifa ya Michezo ya Olimpiki ya Walemavu (KNPC) ilikuwa imeanzisha mchakato wa kupata mbadala wa Mwaniki kuchukua nafasi ya Ogada kwenye Michezo hiyo inayoanza rasmi hapo kesho.
Muga alisema kuwa anafuraha kuwa Ogada hakuwa amejeruhiwa na kwamba Mwaniki yuko nje ya hatari yoyote ijapokuwa anahitaji muda kupona.
Ogada, ambaye ni mlemavu wa macho atashiriki shindano la Tandem Road Racing B1 Jumatano wiki ijayo.
Imetayarishwa na Nelson Andati