SENEGAL KUCHEZA CECAFA
Shirikikisho la mpira la (CECAFA) limethibitisha kuwa Senegal itachukua nafasi ya Congo Brazzaville katika michuano ijayo ya CECAFA ya Mataifa Nne ya Pre-CHAN itakayofanyika Julai 21-27, 2025, Arusha, Tanzania.
Mechi hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Karatu, kwa kushirikisha timu shiriki zikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania na Senegal.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo, Congo Brazzaville ilijiondoa katika michuano hiyo kutokana na changamoto za vifaa. Michuano hiyo ni maandalizi ya michuano ya CAF ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, ambayo itaandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania mwezi ujao.
Awali, mashindano hayo yalipangwa kwa njia ya mtoano, ambapo washindi wa mechi mbili za nusu fainali wangetinga fainali, huku walioshindwa wakiwania nafasi ya tatu.
Walakini, waandaaji wamerekebisha muundo hadi muundo wa duara, ambapo kila timu itacheza mechi tatu.
Timu iliyo na pointi nyingi zaidi mwishoni mwa mashindano itatangazwa kuwa mshindi.
Huku hayo yakijiri, Harambee Stars, ambayo kwa sasa iko kambini katika uwanja wa Kasarani, inazidisha matayarisho ya dimba hilo la kanda.
Kocha Mkuu Benni McCarthy na benchi lake la ufundi wanatarajiwa kurekebisha mbinu na kutathmini kikosi kabla ya kusafiri Tanzania siku zijazo.
Michuano hiyo inaipa Kenya fursa muhimu ya kukifanyia majaribio kikosi chake kabla ya CHAN 2024, huku timu hiyo ikilenga kuimarisha makali yake ya ushindani dhidi ya wapinzani wakubwa wa eneo hilo.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































