WAKENYA HUKOPA MILIONI 500 KILA SIKU, RIPOTI YAFICHUA
Ripoti mpya ya Chama cha Huduma za Kifedha za Kidijitali nchini (DFSAK), imefichua kuwa wakenya hukopa kiwango cha wastani cha shilingi milioni 500 kila siku, kiasi cha Ksh.15 bilioni kila mwezi.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 8, sawa na 16%, hutumia huduma za utoaji mikopo kwa njia ya kidijitali kila mwezi. Hii inaonyesha ongezeko kubwa la utegemezi wa huduma hizi miongoni mwa wakenya, wakichukua mikopo kwa haraka kupitia majukwaa ya kidijitali ili kukabiliana na changamoto za kifedha za kila siku.
Aidha, chama hicho kimeripoti kuwa malalamiko ya watumiaji yamepungua kwa kiasi kikubwa kutoka 4,000 kwa mwezi hadi idadi ndogo zaidi kutokana na kupitishwa kwa kanuni kali za maadili.
Hata hivyo, chama hicho kinashinikiza serikali kutunga sheria zitakazoelekeza utoaji wa mikopo kwa njia ya uwazi na kuwa na mfumo wa kushughulikia ukwepaji wa kulipa madeni.
Imetayarishwa na Mercy Asami
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































