#Business

MSAMAHA WA USHURU WA KRA WAFIKIA KSH 158 BILIONI

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru Nchini, KRA, imetangaza kuwa zaidi ya walipa ushuru milioni 2.9 wamefaidika na Mpango wa Msamaha wa Ushuru ambao ulianza Disemba 27, 2024.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Ushuru, Humphrey Simiyu, tangu uzinduzi wa mpango huo, KRA imekusanya jumla ya shilingi bilioni 10.9 kama malipo ya kodi ya msingi kutoka kwa walipa ushuru waliotumia fursa hiyo kuondoa madeni ya zamani.

Mpango huu wa msamaha unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2025, na unalenga kuwasaidia walipa ushuru kusafisha rekodi zao za ushuru na kurekebisha hali ya kufuata sheria za ushuru nchini.

KRA imeeleza kuwa chini ya mpango huu, walipa ushuru ambao hawana deni la msingi hadi Disemba 31, 2023, watapata msamaha wa moja kwa moja wa riba, faini na adhabu.

Hata hivyo, wale walio na madeni ya ushuru yaliyoanza kuanzia tarehe 1 Januari, 2024 na kuendelea, hawatafaidika na msamaha huo. Watalazimika kulipa kwa ukamilifu deni la msingi, pamoja na riba na adhabu husika.

Imetayarishwa na Mercy Asami

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *