ARSENAL WAJIOKOA NA IKABU, UNITED NAFASI YA 3
Viongozi wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza, EPL, Arsenal, walirejesha mwanya wa pointi 5 kati yao na Manchester City baada ya kushinda pambano la mipira mifu dhidi ya Chelsea hapo jana.
Katika ushindi wa mabao 2-1, mabao yote yalifungwa kutokana na mipira ya kona.
Beki William Saliba aliwaweka Gunners kifua mbele katika dakika ya 21 kutokana na kona ya Gabriel Magalhaes, kabla ya msafara wao wa kuelekea ubingwa wa taji la EPL kutishiwa kusitishwa katika dakika za majeruhi kipindi cha kwanza beki wao Piero Hincapie alipojifunga bao, pia kutokana na kona ya beki wa The Blues Reece James.
Hata hivyo, utovu wa nidhamu ulijitokeza tena katika kikosi cha Chelsea, mara hii Pedro Neto akipokea kadi nyekundu baada ya kadi 2 za njano, ya kwanza kwa kuteta, na ya pili kwa kucheza visivyo.
Arsenal ambao sasa walikuwa wamepunguziwa wapinzani, walitumia fursa hiyo na kujipa bao la pili kupitia kwa beki Jurien Timber kutokana na kona ya Declan Rice.
Kwa sasa Gunners wana pointi 64 kileleni, wakifuatiwa na City walio na pointi 59 kufuatia ushindi wao mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Leeds Jumamosi usiku.
Manchester United waliotoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Crystal Palace, wamechupa hadi nafasi ya 3 juu ya Aston Villa wakiwa na pointi 51, sawa na Villa.
Kichapo cha Chelsea kinawaacha katika nafasi ya 6 kwa pointi 45, pointi 3 nyuma ya Liverpool walio katika nafasi ya 5.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































