#Football #Sports

CHUI WA AFC WAIKWARUZA SHABANA

Klabu ya AFC Leopards iliikwaruza Shabana FC katika mechi ya kusisimua ugani Gusii mjini Kisii kwa kichapo cha mabao 2-1 hapo jana na kuiweka katika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa ligi.

Wenyeji Shabana walitangaza ubabe wao mwanzoni mwa mechi na kuchukua uongozi kupitia kwa fowadi wao Austin Odongo ila Leopards wakadinda kufyata mkia na badala yake kuonyesha kucha zao.

Nahodha Victor Omune aliwarejesha mchezoni katikati mwa kipindi cha pili, baada ya mabadiliko wakati wa mapumziko

Kizaazaa katika kijisanduku cha Shabana kutokana na kona yake James Kinyanjui ilisababisha wenyeji kujifunga dakika za jioni, na kuihakikishia Ingwe ushindi wa mechi 2 mfululizo na mechi 5 mfululizo bila kupoteza.

Nao Shabana FC wanaonolewa na Peter Okidi, sasa wamepoteza mechi 3 mfululizo, na mechi 5 bila ushindi.

Kwa sasa Leopards wana alama 9 katika nafasi ya 5, alama 4 pekee nyuma ya viongozi Kakamega Home Boyz.

Home Boyz walipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya APS Bomet, na kuwaweka kileleni kwa alama 13, alama 3 mbele ya nambari 2 Bidco United waliopata ushindi wa mabao sawa dhidi ya Ulinzi Stars hapo jana.

Mechi zaidi zimeratibiwa hii leo ambapo Murang’a Seal watalenga kuweka muhuri kwenye barua za Posta Rangers, Green Commandos wa Gor Mahia wakimenyana na Mathare United.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

CHUI WA AFC WAIKWARUZA SHABANA

DE BRYUNE AFANYIWA UPASUAJI

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *