MWATSINGWA AIPA SS ASSAD USHINDI DHIDI YA MSA UNITED

SS Assad wamewashinda wenyeji Mombasa United, kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili (NSL) iliyochezwa jana Jumapili katika Uwanja wa Michezo wa Serani, Kaunti ya Mombasa.
Hemed Mwatsingwa alifunga bao pekee la Assad katika dakika ya 15, kwa shuti la chini na kali lililomshinda mlinda lango wa Mombasa United, Kevin Tila, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Nahodha Ali Pinda.
Dakika tano baadaye, mlinda lango wa United, Tila, aliiokoa timu ya nyumbani kwa kutoka nje ya boksi la mita 18 kumzuia mshambuliaji wa Assad, Mohammed Mbaradi, aliyekuwa na nafasi ya wazi ya kufunga kwenye shambulizi la kushtukiza.
United walilazimika kufanya mabadiliko ya mapema dakika 10 kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, wakimleta Ramadhan Mwanzia kuchukua nafasi ya Ateek Zubeir.
Timu ya nyumbani ilienda mapumziko bila hata shuti moja lililolenga goli, lakini walikuwa hatari zaidi katika kipindi cha pili, ingawa hawakufanikiwa kufunga.
Dakika 10 ndani ya kipindi cha pili, United walipata nafasi yao ya kwanza ya maana, ambapo Bernard Odhiambo alipiga shuti kutoka umbali wa mita 30, lakini mlinda lango wa Assad alilipangua mpira huo nje kwa kona.
Imetayarishwa na Janice Marete