CAF YAFUNGUA UCHUNGUZI BAADA YA VURUGU KATI YA ALGERIA, NIGERIA
Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, limetangaza kuwa limefungua uchunguzi na kuonya juu ya uwezekano wa kuchukua hatua za kinidhamu kufuatia tabia iliyoelezwa kuwa isiyokubalika baada ya wachezaji wa Algeria na Nigeria kukabiliana uwanjani mwishoni mwa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Mataifa bingwa ya Afrika, AFCON.
Mvutano ulizuka uwanjani baada ya kipenga cha mwisho cha mechi ya Jumamosi iliyochezwa mjini Marrakesh, ambapo Nigeria iliibuka na ushindi wa mabao 2–0 kupitia magoli ya kipindi cha pili ya Victor Osimhen na Akor Adams.
Hatua zozote za kinidhamu zinaweza kuathiri maandalizi ya Super Eagles wanapojiandaa kwa nusu fainali dhidi ya Morocco itakayochezwa hapo kesho.
Hata hivyo, CAF pia imethibitisha kuwa inachunguza matukio yaliyotokea katika mechi nyingine ya robo fainali ya Ijumaa kati ya wenyeji Morocco na Cameroon.
Morocco ilishinda mechi hiyo 2–0 mjini Rabat, lakini Cameroon walionyesha kutoridhishwa na maamuzi ya marefa, hasa baada ya kunyimwa penalti kwa kosa lililodaiwa kufanywa dhidi ya mshambuliaji wa Manchester United, Bryan Mbeumo, katika kipindi cha pili.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































