HARAMBEE STARS KUJITATHMINI DHIDI YA SENEGAL
Timu ya taifa Harambee Stars itaendeleza safari yake ya kujiimarisha dhidi ya Senegal leo jioni katika mechi yake ya mwisho ya kirafiki katika kipindi cha likizo ya kimataifa itakayochezwa nchini Uturuki.
Timu zote zinakutana kufuatia kichapo kwenye mechi zao za kirafiki za kwanza, Stars wakibamizwa 1-0 na Equatorial Guinea huku Senegal wakimenywa na Brazil 2 mtungi.
Senegal wakitumia mechi ya leo kujipima nguvu kabla ya kipute cha AFCON mwezi ujao nchini Morocco na kombe la dunia nchini Marekani mwaka ujao, Stars wanajiandaa kwa kipute cha AFCON mwaka 2027.
Kocha mkuu wa Stars Benni McCarthy, anasema kikosi hicho kitatumia kila fursa kujiimarisha na kushindana kisawasawa katika mashindano hayo ya bara.
Baadhi ya wachezaji akiwemo kiungo Duke Abuya, wamesema mechi ya leo dhidi ya Senegal ni ya kupima maendeleo ya kikosi hicho katika safari yake ya kujinoa.
Mechi hiyo itachezewa katika uwanja wa Mardan, jijini Antalya saa 6pm.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































