KPA YAWAKA MOTO WA VIKAPU
Klabu ya mchezo wa vikapu KPA imeendeleza msururu wake wa matokeo bora katika dimba la Ligi ya wanawake barani Afrika mwaka huu toleo la FIBA Zone 5, ikiwabebesha Gladiators wa Burundi vikapu 100-42 katika pambano lao la 3 kwenye Pool A ugani Nyayo.
Wanabandari hao ambao hajawapoteza mikononi mwa timu yoyote katika dimba hilo, walitawala mchezo wao dhidi ya Gladiators kutokea mwanzo hadi mwisho na kuandikisha ushindi huo kwenye robo zote 4.
Mabingwa hao wa ligi ya kitaifa walianza kwa kishindo, wakiibuka washindi katika robo ya kwanza kwa pointi 22-06, kabla ya ushindi dhabiti wa pointi 26-05 na hivyo kuelekea mapumziko wakiwa mbele kwa pointi 48-11.
Sajili mpya Betty Kananu alionyesha mchezo wa aina yake, akiwapa wanabandari hao pointi 27 na kuwaweka kwenye mkondo wa kutwaa ushindi.
Nao raia 3 wa kigeni akiwemo Alima Doumbia wa Ivory Coast, Ifunanya Okoro wa Nigeria na Msenegali Aminata Ly walishirikiana na kuipa klabu hiyo pointi 40.
Ushindi huo wa jana unaiweka KPA kileleni mwa Pool A kwa pointi 6, sawa na APR ya Rwanda, kutokana na ushindi wao wa pointi 70-50 dhidi ya Magic Stormers wa Uganda.
KPA na APR wanamenyana leo 7:30 usiku katika pambano la aina yake kuamua kiongozi wa Pool A kabla ya awamu ya mwondoano.
Klabu 2 za kwanza kutoka dimba hilo zitafuzu kwa raundi ya mwosho jijini Cairo, Misri mwezi ujao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































