KENYA PRISON YAPATA SURA MPYA

Mshambulizi mahiri wa Kenya Prisons Meldina Sande, mshambuliaji wa DCI Jemimah Siang’u na libero wa KCB Lincy Jeruto wameondolewa kwenye kikosi cha mwisho cha Malkia Strikers kitakachoelekea kwa michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Watatu hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Malkia Strikers kilichofungwa 3-0 na Puerto Rico katika robo fainali ya Kombe la Challenger wiki jana nchini Ufilipino na hawakubahatika kuwa kwenye kikosi cha mwisho cha kocha Japheth Munala.
Mshambuliaji mkali wa pembeni Pamela Adhiambo, ambaye alifunga pointi 22 dhidi ya Puerto Rico yuko ndani pamoja na mshambuliaji kutoka Ugiriki Veronicah Adhiambo na Sharon Chepchumba ambaye alirejea KCB mapema mwaka huu baada ya kucheza kwa miezi sita PAOK Thessaloniki nchini Ugiriki. .
Mchezaji wa Kenya Pipeline Leonidah Kasaya ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi ambaye atakuwa akishiriki kwa mara ya pili kwenye Michezo ya Olimpiki baada ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020.
Kikosi hicho chenye wachezaji 13 kitakuwa na nahodha na Trizah Atuka ambaye alichukua usukani kutoka kwa Mercy Moim, na naibu wake ni Edith Wisa.
Malkia Strikers wataondoka nchini wiki hii kwa mazoezi ya wiki mbili ya kiwango cha juu huko Miramas kabla ya kuelekea Paris kwa michezo ya Olimpiki itakayoanza Julai 26.
Imetayarishwa na Nelson Andati