HUDUMA BORA ZA MAHAKAMA KUZINDULIWA KISUMU NA NYANZA
Wakazi wa Kisumu na maeneo ya Nyanza wanatarajiwa kunufaika na huduma bora zaidi za mahakama kufuatia uzinduzi wa huduma za pamoja za mabaraza ya usuluhishi (Tribunals Shared Services) unaotarajiwa kufanywa leo asubuhi na Jaji Mkuu Martha Koome, hafla ambayo imeratibiwa kufanyika katika ofisi za Lake Victoria South Water Works Development Agency, Nyalenda, kuanzia saa 9:30.
Mbali na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, mpango huu pia utawapatia wananchi fursa ya kupata huduma kutoka kwa mabaraza mbalimbali katika eneo moja, msaada wa kidijitali kama vile uwasilishaji wa kesi kwa njia ya mtandao (e-filing), vikao vya mtandaoni, majukwaa ya kidijitali, na kituo kimoja cha taarifa kwa zaidi ya mabaraza 26.
Idara ya Mahakama imepitisha mfumo wa huduma za pamoja kwa mabaraza haya, ambao ni mkakati wa kuunganisha huduma kuu kama vile TEHAMA, miundombinu, fedha, ugavi, mawasiliano, na rasilimali watu chini ya mfumo mmoja.
Imetayarishwa na Janice Marete
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































