AFCON 2027: WABUNGE WAPINGA PENDEKEZO LA KUONGEZA BAJETI
Kamati ya michezo katika bunge la kitaifa imekatalia mbali pendekezo la wizara ya michezo kutaka mgao wa bajeti ya maandalizi ya kombe la taifa bingwa barani Afrika AFCON 2027 uongezwe.
Haya yanajiri licha ya kuibuka kwamba Kenya haijalipa ada yake ya lazima ya shilingi bilioni 3.5 zinazohitajika ili kuwa mwenyeji wa dimba hilo.
Chini ya mwenyekiti wake mbunge wa Webuye West Dan Wanyama, kamati hiyo imepinga pendekezo la kuongeza mgao huo kutoa shilingi bilioni 3.5 hadi bilioni 5, ikisema sababu zilizotolewa hazitoshi.
Badala yake, kamati hiyo imependekeza kupunguzwa kwa bajeti hiyo ikizingatiwa kuwa dimba hilo litaandaliwa katika mataifa matatu ikiwemo Kenya, Uganda na Tanzania.
Kulingana na katibu katika wizara hiyo Elijah Mwangi, Uganda na Tanzania tayari yametuma ada zao kwa CAF, wakitaka wabunge kuhakikisha mgao huo unajumuishwa kwenye bajeti ya ziada ili kuiwezesha Kenya kuafikia vigezo vya CAF.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































