STARLETS WAINGIA KAMBINI
Kikosi cha wanasoka 35 wa timu ya taifa ya soka kwa akina dada chini ya miaka 17 maarufu Junior Starlets kitaingia kambi ya mazoezi ya majuma mawili ugani Utalii Nairobi kuanzia hapo kesho kujiandaa kushiriki kombe la dunia mwezi ujao nchini Dominican Republic.
Kocha mkuu Mildred Cheche aliyewaongoza warembo hao kufuzu kwa kombe hilo la dunia litakaloanza Oktoba tarehe 16 hadi Novemba tarehe tatu, kwa kuwalemea Burundi jumla ya mabao 5-0 katika raundi ya nne na ya mwisho ya kufuzu mwezi Juni mwaka huu, alikitaja kikosi ghafi cha wachezaji hao 35 wiki moja imepita kilichotinga kambini kabla ya kupunguzwa.
Warembo hao watakuwa kambini hadi Septemba tarehe 10 watakapoondoka kuelekea kwenye kambi ya kimataifa nchini Uhispania kabla ya kuunganisha safari yao ya kwenda Jamuhuri ya Dominica Oktoba tarehe nne kushiriki taji hilo.
Kwenye taji hilo la ulimwengu, Starlets wamo kwenye kundi C pamoja na Korea DPR, Mexico na Uingereza.
Timu hiyo aidha imepigwa jeki pakubwa baada ya wachezaji wanane waliotarajiwa kukalia mtihani wao wa kitaifa wa KCSE mwaka huu katika tarehe inayolandana na ubingwa huo kupangiwa mtihani speheli na baraza la mtihani nchini KNEC ili kuwakilisha taifa kwenye kombe la dunia.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 

























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































