GOR WAREJESHA UONGOZI WA POINTI 6 KILELENI
Miamba wa soka nchini Gor Mahia walirejesha uongozi wa pointi 6 kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya soka nchini, KPL, kufuatia ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya wanabenki wa KCB.
Ushindi wa Green Commandos ukijiri baada ya AFC Leopards kupunguza mwanya wa pointi kwa kuwachabanga Posta Rangers 2-1, uliihakikishia Gor mfululizo wa mechi 11 bila kuonja kichapo.
Kufikia kipindi cha mapumziko, K’Ogalo walikuwa wamefanya asilimia kubwa ya kazi kwa kuwaadhibu KCB kwa makosa yao, Enock Morrison akiwapa uongozi katika dakika ya 24 kabla ya Sharif Musa kuweka la pili dakika 4 baadaye.
Licha ya utelelezi kutokana na mvua katika uwanja wa Nyayo, washambulizi wa K’Ogalo waliendelea kuitaabisha safu ya ulinzi ya KCB, Samuel Kapen akimaliza matumaini ya wanabenki kurejea mchezoni kuelekea mapumzikoni.
Gor wanaongoza kwa pointi 46 baada ya kusakata mechi 21, nao Ingwe wakifuata kwa pointi 40 baada ya mechi 20.
Shabana FC wanashikilia nafasi ya 3 kwa pointi 37 huku Kakamega Homeboyz wakiwa katika nafasi ya 4 kwa pointi 34.
Mabingwa watetezi Police FC walioandikisha sare ya 3 mfululizo, wanajitetea wakiwa nafasi ya 7 na pointi 31 baada ya mechi 21.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































